Friday, 11 October 2013

NI MBABE MPYA MWENYE MVUTO BAADA YA LENNOX LEWIS KATIKA NDONDI ZA UZITO WA JUU, ANAITWA JOSHUA, ANGALIA ALIVYOMUADHIBU MTALIANO

TANGU kustaafu kwa Lennox Lewis hajatokea mbabe mwingine mwenye mvuto katika ndondi za uzito wa juu, lakini Jumamosi usiku Anthony Joshua alionyesha anaweza kurudisha raha katika masumbwi ya uzito wa juu. Mbabe huyo wa London na mshindi wa Medali ya Dhahabu ya Olimpiki, alianza vyema ndondi za kulipwa kwa kumpiga mpinzani wake Emanuele Leo kwa Knockou (KO) Raundi ya kwanza ukumbi wa O2 Arena. Chali, kwisha kazi : Anthony Joshua (kushoto) akiwa amemdondosha Emanuele Leo katika Raundi ya kwanza kwenye pambano lake la kwanza la ndondi za kulipwa Tayari anatabiriwa kuwa Lennox Lewis mwingine na kutamba katika ulimwengu wa ndondi hadi kuwa bingwa asiyepingika wa uzito wa juu duniani.

Kazi nyepesi: Joshua alianza vyema maisha ya ndondi za kulipwa

Ana ngumi nzito Anatisha kijana: Joshua atarejea ulingoni baadaye mwezi huu ili kujijenga zaidi Mwisho, konde la nguvu la Joshua limetua kichwani kwa jamaa

Thursday, 26 September 2013

BEKI LA NGUVU KAZE GILBERT NA MSHAMBULIAJI HATARI TAMBWE WAREJEA KAZINI SIMBA SC

BEKI Kaze Gilbert aliyeumia nyonga Jumamosi Simba SC ikimenyana na Mbeya City na kutoka sare ya 2-2 katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, anatarajiwa kurejea mazozini leo baada ya kupona.
Aidha, Mrundi mwenzake Amisi Tambwe aliyeumia pia nyama katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, naye anatarajiwa kuanza mazoezi leo.
Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mbali na Warundi hao wawili waliosajiliwa kutoka Vital’O ya Burundi, majeruhi mwingine ni kiungo Henry Joseph ambaye anasumbuliwa na maumivu ya goti.

Warundi wawili; Kaze Gilbert na Amisi Tambwe wote wanarejea mazoezini leo


“Henry bado kidogo, nadhani kuanzia kesho tunaweza kujua anaweza kuanza lini mazoezi. Lakini Kaze na Tambwe wote tunawatarajia leo wataanza mazoezi,”alisema.

MANJI AWATULIZA WACHEZAJI YANGA SC, AWAAMBIA HANA NOMA NAO, AMVUTA NGASSA PEMBENI WAYAMALIZA 'KIKUBWA'

MWENYEKITI wa Yanga SC, Alhaj Yussuf Mehboob Manji amewaambia wachezaji wa timu hiyo kwamba hana matatizo nao kwa matokeo ya awali ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na amewataka waelekeze nguvu zao katika mechi zijazo.
Yanga imeambulia pointi sita katika mechi tano za awali za Ligi Kuu ya Vodacom, kutokana na sare tatu, kushinda moja na kufungwa moja, hivyo kuachwa kwa pointi tano kileleni na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
Jana Manji alikutana kwa chakula cha jioni na wachezaji wa timu hiyo katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam akiwa ameambatana na Makamu wake Mwenyekiti, Clement Sanga, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Isaac Chanji na Mjumbe wa Sekretarieti, Patrick Naggi.


Manji akipeana mkono na Chuji alipokutana na wachezaji hao mwaka jana.

Katika kikao hicho, Manji aliwaambia wachezaji wa Yanga hamlaumu yeyote kwa matokeo hayo, kwani ligi bado mbichi, ila akawataka waunganishe nguvu zao kuelekea mechi zijazo, ili kurejesha ushindi na furaha klabuni.
Pamoja na hilo, Manji alizungumzia suala la madai ya baadhi ya wachezaji ya fedha za usajili na akaliweka sawa kwa wale ambao walikuwa wanadai kuwawekea utaratibu wa malipo haraka, jambo ambalo Naggi ametakiwa kuhakikisha analishughulikia mara moja.
Aidha, Manji baada ya kikao cha pamoja na wachezaji wote, alimvuta pembeni Mrisho Ngassa kujadiliana naye faragha.

Haikujulikana mara moja Manji alizungumza nini na Ngassa, lakini inaweza kuwa kuhusu deni analotakiwa kuilipa Simba SC, Sh. Milioni 45 kwa kosa la kusaini Mikataba na timu mbili. Ngassa alifungiwa mechi sita za mashindano na kutakiwa kurejesha fedha alizochukua Simba SC Sh. Milioni 30 pamoja na fidia ya Sh Milioni 15.

NGASSA AGOMA KUSAINI HATI YA YANGA SC KUMLIPIA DENI LA SIMBA SC, APATA BONGE LA OFA UARABUNI

MRISHO Khalfan Ngassa amepata timu ya Oman inayotaka kumnunua kutoka Yanga SC pamoja na kulipa deni la Simba SC, Sh. Milioni 45, lakini uongozi wa klabu yake kama unamuwekea kauzibe hivi.
Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata juu ya sakata la Ngassa na Yanga ni kwamba, mchezaji huyo amepata timu inayotaka kumnunua moja kwa moja, ikiwa tayari kutoa kiasi cha Sh. Milioni 100, ambazo zitalipa deni la Simba na nyingine kulipwa Yanga ambao wana Mkataba naye kwa sasa.
Hata hivyo, wakati Yanga ikimzuia Ngassa kwenda Oman, nayo inaonekana kusuasua kumilipia deni la Simba SC.
Habari zinasema Yanga wametaka kumsainisha Ngassa Mkataba wa kumlipia deni, lakini amegoma kuusaini kwa kuhofia kurudia kosa alilofanya kusaini Mkataba na Simba SC ambao hakuuelewa.

Mpenzi wa Yanga; Mrisho Ngassa amegoma kusaini kichwakichwa fomu za kulipiwa deni

“Ngassa ameshituka sasa hivi, amegoma kusaini huo Mkataba wa kulipiwa deni, kwanza hadi aupeleke kwa Wakili wake akaupitie. Unajua Simba walimuambia anasaini kukubali kucheza kwa mkopo, kumbe anasaini Mkataba mpya, sasa amekuwa mjanja sana sasa hivi,”kilisema chanzo.
Chanzo hicho kimesema kwamba, Yanga inataka kumlipia Ngassa deni na kuongeza miaka miwili katika Mkataba wake kutoka miwili ya sasa, lakini yeye mwenyewe mchezaji amependekeza alipiwe deni hilo na baada ya hapo atakuwa anakatwa kwenye mshahara wake.
Hadi sasa Ngassa hajasaini hati aliyotakiwa kusaini alipiwe deni hilo, maana yake kuna hatari akashindwa kuanza kucheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ikumbukwe Ngassa alifungiwa mechi sita za mashindano kwa kosa la kusaini Mikataba na timu mbili, Simba na Yanga SC. Pamoja na adhabu hiyo aliyomalizia Jumapili, Ngassa alitakiwa kurejesha fedha alizochukua Simba SC Sh. Milioni 30 pamoja na fidia ya Sh Milioni 15, jumla Milioni 45.

MAMLAKA MWANZA ZAAHIDI NYASI BANDIA NYAMAGANA

MAMLAKA za Mkoa wa Mwanza zimesema zitatimiza ahadi yao ya kuchangia dola 118,000 za Marekani (zaidi ya sh. milioni 190) ili kukamilisha mradi wa kuweka nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza kabla ya Oktoba 15 mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo pamoja na Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula wametoa ahadi hiyo wakati wa kikao kati yao na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga kilichofanyika leo (Septemba 25 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF.


Rais wa TFF, Leodegar Tenga (wa pili kushoto) akiwa na ujumbe wa Mkoa wa Mwanza ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Evarist Ndikilo ulipomtembelea katika ofisi za TFF jana. Wa tatu kutoka kushoto ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula akifuatiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida Hassan.

Wakuu hao wa Mwanza katika kikao hicho pia walifuatana na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida Hassan.
TFF ilipeleka mradi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wa Goal Project IV wa nyasi bandia wa dola 500,000 za Marekani katika Uwanja wa Nyamagana.
Mradi huo ulipelekwa huko baada ya Mkoa wa Mwanza kuahidi kuchangia dola 118,000 ili kukamilisha thamani ya mradi mzima ambayo ni dola 618,000 za Marekani. Wamiliki wa uwanja huo ni Jiji la Mwanza.

Goal Project I ilitumika kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya TFF (technical centre), Goal Project II nyasi bandia Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume wakati Goal Project III iliweka nyasi bandia katika Uwanja wa Gombani ulioko Pemba, Zanzibar.

RHINO RANGERS YAISHUSHA YANGA LIGI KUU BAADA YA KUICHAPA ASHANTI UNITED LEO TABORA

RHINO Rangers imepata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, baada ya leo kuilaza Ashanti United mabao 2-0 Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora.
Kwa ushindi huo, timu hiyo ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) imefikisha pointi saba na kupanda hadi nafasi ya nane ikiwashusha kwa nafasi moja, mabingwa watetezi, Yanga SC.


Juu ya mabingwa; Rhino leo wameishusha Yanga kwa nafasi moja

Katika mchezo huo, mabao ya Rhino yalifungwa na Kamana Salum dakika ya 26 na Hussein Abdallah dakika ya 64.
Ligi hiyo itaendelea Jumamosi wakati, Yanga SC itakapomenyana na Ruvu Shootings Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Rhino Rangers wakiikaribisha Ashanti United Mwinyi, Tabora.

Mechi nyingine zitapigwa Jumapili, Simba SC ikishuka dimbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na JKT Ruvu, Rhino Rangers na Kagera Sugar Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora, Mbeya City na Coastal Union Sokoine, Mbeya, Mgambo JKT na JKT Oljoro Mkwakwani, Tanga na Ashanti United na Mtibwa Sugar, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

MAN UNITED YAICHAPA LIVERPOOL 1-0 KOMBE LA LIGI

MACHO yote yalikuwa kwa Luis Suarez baada ya kurejea Liverpool kufuatia kumaliza adhabu yake ya mechi 10, lakini Javier Hernandez akaiteka shoo kwa bao lake pekee lililoipeleka Manchester United Raundi ya Nne ya Kombe la Ligi, maarufu kama Capital One.
Hatimaye Suarez alicheza mechi yake ya kwanza ya msimu mpya baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake ya kumng'ata beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic msimu uliopita.
Na wakati mshambuliaji huyo wa Uruguay alizomewa na mashabiki Uwanja wa Old Trafford, alikuwa ni Chicharito aliyepoza maumivu ya David Moyes kufuatia kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa wapinzani, Manchester City katika Ligi Kuu Jumapili.
Liverpool ilitawa sehemu kubwa ya mchezo na Daniel Sturridge alipoteza nafasi kadhaa nzu za kufunga, lakini Hernandez hakufanya makosa alipopata nafasi dakika ya 46.
Wayne Rooney, ambaye ndiye mchezaji bora zaidi kwa United hivi sasa, alipiga kona nzuri baada ya mapumziko na Hernandez akaunganisha nyavuni.
Kikosi cha Manchester United kilikuwa: De Gea, Rafael Da Silva, Smalling, Evans, Buttner, Jones, Giggs, Nani, Rooney, Kagawa na Hernandez.
Liverpool: Mignolet, Toure, Skrtel, Sakho, Jose Enrique, Gerrard, Lucas, Henderson, Suarez na Moses, Sturridge. 


Shujaa: Javier Hernandez akishangilia baada ya kufunga bao pekee la Manchester United Uwanja wa Old Trafford